Rais William Ruto ameahidi kwamba serikali yake itaboresha barabara ya kutoka Nairobi kuelekea Nakuru na kuifanya kuwa ya safu mbili mwaka ujao ili kupunguza msongamano wa magari.
Rais Ruto ambaye alikuwa akizungumza katika Kanisa la Kipkorgot AIC kaunti ya Uasin Gishu alisema mradi huo utaendelezwa hadi Malaba kwa ajili ya kuboresha usafiri na biashara.
Tangazo hili linawadia baada ya malalamishi mengi kutoka kwa wanaotumia barabara hasa msimu huu wa sherehe wakati msongamano mkubwa ulichelewesha safari zao kwa masaa mengi.
Rais lisema pia kwamba ni mpango wa serikali wa kubadilisha nchi hii katika hatua inayonuiwa kukuza uchumi na kupunguza gharama ya chakula.
Alisema marekebisho yanayoendelea katika kama vile kilimo na uchumi yameleta ufanisi akisema nchi hii haijaagiza mahindi mwaka huu kutokana na uzalishaji ulioimarishwa.
Kiongozi wa nchi alisema marekebisho hayo yameimarisha idadi ya watalii wanaozuru taifa hili kutoka milioni- 1.9 mwaka uliopita hadi milioni-2.5 mwaka huu.
Kuhusu chanjo ya mifugo, Rais alisema mpango huo utatekelezwa licha ya upinzani kutoka kwa baadhi ya wanasiasa na matabibu wa mifugo.
Kwa mara nyingine kiongozi wa nchi alihimiza wazazi na kanisa kukuza watoto wao kimaadili kwa ushirikiano na kanisa.
Kulingana naye, kukosa kukuza watoto na vijana kimaadili husababisha ongezeko la visa vya uhalifu huku akihimiza jamii kukumbatia ushirikiano jumuishi kukabiliana na jinamizi la uhalifu na mauaji ya kikatili ya wanawake kwa jumla.