Rais William Ruto ameahidi kukipa Chuo Kikuu cha Baraton shilingi milioni 60 ambazo zitasaidia katika ujenzi wa vifaa zaidi chuoni humo.
Akizungumza alioongoza mahafali ya 42 ya chuo hicho jana, kiongozi wa nchi alikisifia kwa kuwa cha kwanza kutoa kozi ya shahada ya uuguzi nchini na kwamba waliosomea huko ni kati ya wahudumu bora wa sekta ya afya nchini.
Wakati wa mahafali ya jana, wanafunzi 1,267 walifuzu na shahada za kozi mbalimbali huku Rais Ruto akitunukiwa shahada ya heshima ya uzamivu katika masuala ya uongozi na huduma kwa jamii.
Kiongozi wa nchi alifafanua kwamba alipokea ombi la ufadhili kutoka kwa serikali kwa chuo kikuu cha Baraton kinachoendeshwa na kanisa la kiadventista nchini.
“Ninaelekeza wizara ya elimu itoe ruzuku ya milioni 60 kwa chuo hiki ili kiweze kukamilisha ujenzi huo,” alisema Ruto wakati wa hotuba yake.
Rais alipongeza waliofuzu akiwataka watumie elimu waliyopokea katika kuboresha nchi hii.
Waziri wa Elimu Migosi Ogamba kwa upande wake alivitaka vyuo vikuu kujianzisha upya na kujiimarisha ili viweze kijisimamia.
Prof. Jackson Msafiri Mamba alisimikwa kama Naibu Chansela wa Chuo Kikuu cha Baraton na anachukua mahali pa Profesa Philip Maiyo ambaye ameshikilia wadhifa huo kwa muda wa miaka 10.
Rais Ruto alidhihirisha imani yake katika uwezo wa Mamba akisema ana imani kwamba atainua taasisi hiyo ya elimu ya juu.