Rais William Ruto ameelekeza taasisi za serikali zifutilie mbali mikataba miwili maarufu ya Ushirikiano wa Umma na Binafsi yaani “Public Private Partnership – PPP” kutokana na madai yanayoibuka ya ufisadi.
Mikataba hiyo inahusisha mchakato wa upanuzi unaoendelea wa wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) na mradi wa usambazaji umeme wa KETRACO uliohitimishwa hivi karibuni.
Katika hotuba yake kuhusu hali ya taifa katika bunge, Ruto alisisitiza dhamira ya serikali yake ya uwazi na uwajibikaji kama ilivyoelezwa katika Kifungu cha 10 cha Katiba.
“Nimeeleza awali, na naeleza tena leo, kwamba mbele ya ushahidi usiopingika au habari za kuaminika kuhusu ufisadi, sitasita kuchukua hatua mwafaka,” Rais alisema.
Maelekezo hayo yanafuatia habari mpya kutoka kwa taasisi za uchunguzi na ufahamu kutoka kwa mataifa washirika, ambayo yalisisitiza hitaji la hatua za haraka ili kulinda rasilimali za umma.
Ruto aliagiza Wizara ya Uchukuzi na ile ya Nishati kufutilia mbali ushirikiano wao katika mikataba hiyo na kuanzisha mchakato wa kuleta washirika wengine mbadala.
Hatua hii ya ujasiri inaashiria juhudi za serikali za kuimarisha vita dhidi ya ufisadi na kurejesha imani ya umma katika miradi ya serikali hasa ile inayohusisha fedha nyingi.
Hatua hiyo inajiri wakati ambapo bilionea wa India Gautam Adani na washirika wake wengine wakuu wameshtakiwa mjini New York nchini Mrekani kwa kuhusika katika sakata ya utapeli wa mabilioni ya dola kwa mujibu wa kitengo cha sheria nchini Marekani.