Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesisitiza kwamba bendera ya Urusi haifai kupeperushwa kwenye michezo ya Olimpiki mwaka 2024 ambayo itaandaliwa katika nchi yake. Anasema hilo halifai hasa wakati huu ambapo Urusi inatekeleza kile alichokitaja kuwa uhalifu wa kivita.
Urusi ilivamia Ukraine Februari 2022 vita ambavyo vinaendelea hadi sasa na vimesababisha vifo vya wengi, wengi kupoteza makazi na mali nyingi kuharibiwa.
Alipoulizwa iwapo wanariadha raia wa Urusi wanaweza kushiriki michezo ya Olimpiki kama wanariadha huru, Macron alisema kwamba Ufaransa kama nchi andalizi haina uwezo wa kuchagua washiriki na hilo ni jukumu la kamati ya kimataifa ya Olimpiki.
Kiongozi huyo wa Ufaransa alisema ana imani katika Rais wa kamati ya kimataifa ya Olimpiki Thomas Bach kwamba atafanya maamuzi stahiki kuhusu suala hilo.
Wanariadha wa nchi za Urusi na Belarus wamekuwa wakijipata pabaya katika mashindano ya kimatafa ya michezo tangu Urusi ivamie Ukraine.
Kamati ya kimataifa ya Olimpiki imekuwa ikipendekeza kwamba wanariadha wa nchi hizo mbili washiriki kama wanariadha huru wanaotumia bendera isiyo ya nchi yoyote baada ya kutimiza masharti fulani kama vile kudhibitisha kwamba hawajaunga mkono vita vya Ukraine moja kwa moja.
Macron hata hivyo anatilia shaka uwezo wa kamati hiyo kutofautisha kati ya wanariadha waliounga mkono vita vya Ukraine na ambao hawajawahi kuviunga mkono.
Alisema ni sharti kamati ya kimataifa ya Olimpiki ifanye uamuzi ambao utakuwa wa haki kwa watu wa Ukraine na ulimwengu wote.
Ufaransa itaandaa michezo ya Olimpiki mwaka 2024 kati ya Julai 26 na Agosti 11.