Rais Lula asema Rais Putin hatakamatwa akizuru Brazil

Marion Bosire
2 Min Read

Rais wa Brazil Luiz Inacio Lula da Silva amesema kwamba kiongozi wa nchi ya Urusi Vladimir Putin hatakamatwa nchini Brazil iwapo atahudhuria kongamano la nchi 20 zilizo na uwezo mkubwa kiuchumi almaarufu G20. Kongamano la mwaka ujao la kundi la G20 litaandaliwa nchini Brazil.

Lula alizungumza na wanahabari pembezoni mwa kongamano la mwaka huu la G20 jijini Delhi nchini India ambapo alifafanua kwamba Putin ataalikwa kwa kongamano la mwaka ujao la kundi la G20.

Alisema akiwa Rais wa Brazil Putin hawezi kukamatwa katika himaya ya nchi yake.

Alipongeza kwamba yeye mwenyewe anapanga kuhudhuria mkutano wa kundi la nchi zinazostawi linalojulikana kama BRICS huko Urusi kabla ya kongamano la jijini Rio.

Matamshi ya Rais Lula yanatokana na hatua ya mahakama ya kimataifa ya jinai ICC ya kutoa kibali cha kumkamata Rais wa Urusi Vladimir Putin kwa makosa ya kivita ya kuondoa kinyume cha sheria watoto kutoka taifa la Ukraine.

Urusi imekana madai kwamba wanajeshi wake wametekeleza makosa ya kivita au kutwaa watoto wa Ukraine kwa lazima.

Putin amekuwa akikosa kuhudhuria mikutano ya kimataifa na hakuwepo kwenye kongamano la India na G20. Aliwakilishwa na waziri wa mambo ya nje Sergey Lavrov.

Brazil ni mojawapo ya nchi ambazo zilikubali sheria ya Roma ambayo ilisababisha kubuniwa kwa mahakama ya ICC.

Nchi zinazokubaliana na sheria hiyo ya Roma zinatakiwa kukamata yeyote ambaye kibali cha kumkamata kimetolewa na mahakama ya ICC na kumwasilisha huko.

Jumamosi mataifa wanachama wa kundi la G20 yaliidhinisha tamko ambalo halilaumu Urusi kwa vita vinavyoendelea nchini Ukraine lakini yakaonya nchi zote dhidi ya kutumia nguvu kunyakua himaya.

Share This Article