Rais mstaafu Uhuru Kenyatta amewatakia kila la kheri wakenya huku akiwaombea amani na umoja anapoadhimisha miaka 63 tangu kuzaliwa kwake.
“Siku hizi mimi siongei jameni, lakini ninawatakia wakenya wote amani na umoja. Tujue sisi wote ni binadamu, tuna mahitaji, tuwache mambo ya kuzozana, kuingililiana, bali tushikane na tupendane kama wakenya ndipo tuweze kusonga mbele kwa pamoja.” alisema Rais huyo wa nne wa jamhuri ya Kenya.
Alikuwa akizungumza kwenye mahojiano na kituo kimoja cha redio humu nchini ambapo alifurahisha wasikilizaji alipoomba wimbo uitwao “‘I Got You Baby” wa UB40 umwendee mke wake Margaret.
Siku yake ya kuzaliwa mwaka huu ilimpata akiwa jijini Abidjan nchini Côte d’Ivoire, ambapo alikuwa anahudhuria mkutano wa 15 wa kiwango cha juu wa Umoja wa Afrika unaolenga kustawisha amani na Udhabiti barani humu.
Kiongozi huyo alisema katika miaka ya awali alisherehekea siku hiyo ya kuzaliwa na familia.
Kenyatta alionekana hadharani huko Abidjan baada ya muda mrefu huku wakenya wakikisia hali yake mitandaoni huku wakishangaa aliko.