Rais afafanua kuhusu tukio la DRC

Marion Bosire
2 Min Read

Rais William Ruto amefafanua kuhusu kilichotokea jijini Nairobi kuhusu Jamhuri ya Demokrasia ya Cong, DRC ambapo muungano wa waasi na makundi ya kijamii na kisiasa wa nchi hiyo ulibuniwa.

Akijibu maswali ya wanahabari jana jioni katika Ikulu ya Nairobi, kiongozi wa nchi alisema kwamba alikosa kuchukua hatua kwa sababu DRC ni taifa huru.

Alisema pia kwamba Kenya ni taifa ambalo lina uhuru wa kuchagua ndiyo sababu viongozi hao wa waasi na upinzani nchini DRC waliweza kukutana na kutangaza maafikiano yao jijini Nairobi.

Ruto alisema iwapo nchi hiyo inaonelea kwamba kumwondoa balozi wake nchini ndio suluhisho, yeye hawezi kuingilia.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje nchini DRC Alain Tshibanda, alitangaza hatua ya kuondolewa kwa mabalozi wa nchi hiyo kutoka Kenya na Tanzania kupitia mtandao wa X Jumamosi.

Balozi wa DRC nchini Tanzania anasemekana kuitwa kwa sababu nchi hiyo ina makao makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, EAC ambayo DRC ni mwanachama.

Mwenzake wa Kenya anasemekana kuitwa na wizara hiyo mjini Kinshasa kwa majadiliano.

Ijumaa iliyopita, wanasiasa wakuu wa upinzani nchini DRC na wawakilishi wa makundi kadhaa likiwemo lile la waasi la M23 ambalo limeteka eneo kubwa Mashariki ya Congo, walizindua muungano kwa jina “Congo River Alliance” jijini Nairobi.

Website |  + posts
Share This Article