Kinara wa chama cha ODM Raila Odinga sasa anasema chama hicho kitaamua mwelekeo wake katika uchaguzi mkuu wa 2027 wakati mwafaka.
Raila hajafutilia mbali uwezekano wa chama kicho kuwasilisha mgombea urais kwenye uchaguzi huo.
Kulingana naye, chama cha ODM kilitia saini Mkataba wa Maelewano (MoU) na chama tawala cha UDA kushirikiana nacho katika kuunda serikali jumuishi hadi mwaka 2027.
“Hatujapitisha azimio lolote kama chama kuamua tutakavyoenda kwenye uchaguzi mkuu mwaka 2027. Kwa hivyo popote ulipo, usiahidi mambo mengine ambayo hayajapitishwa na chama. Wacha hayo mambo yajadiliwe kwanza,” alisema Raila wakati akiwahutubia wabunge wa chama cha ODM mjini Machakos leo Jumatatu.
“Sisi ni ODM. Nani alikwambia kwamba ODM haitawasilisha mgombea urais mwaka 2027? Nani amekwambia?”
Akizungumza wakati wa Kongamano la Ugatuzi la mwaka huu lililoandaliwa katika kaunti ya Homa Bay mwezi Agosti, Raila alionekana kuashiria kwamba chama chake cha ODM kitamuunga mkono Rais William Ruto kugombea muhula wa pili kwenye uchaguzi wa mwaka 2027.
Mtazamo huo umeungwa mkono na baadhi ya wanachama wa ODM, hasa wabunge na mawaziri kutoka ngome yake ya kisiasa ya eneo la Nyanza.
Hususan, Waziri wa Fedha John Mbadi na mwenzake wa Nishati Opiyo Wandayi wamekuwa mstari wa mbele kuelezea kuwa ODM itasimama sako kwa bado na Rais Ruto kwenye uchaguzi mkuu ujao.
Mbadi na Wandayi ni wanachama wa ODM walioambulia nafasi za uwaziri kufuatia kuundwa kwa serikali jumuishi.
Wengine ni Waziri wa Vyama vya Ushirika Wycliffe Oparanya na mwenzake wa Madini Hassan Joho.