Kinara wa ODM Raila Odinga ameonekana kuchukua hatua zinazolenga kuzuia kutimuliwa kwa Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja madarakani.
Raila akifanikiwa kuwaleta pamoja wawakilishi wadi wa chama cha ODM na Gavana Sakaja kwa lengo la kusuluhisha tofauti kati yao.
Mwakilishi wadi wa Kileleshwa Robert Alai, aliyechaguliwa kwa tiketi ya ODM, alikuwa akiongoza juhudi za kumtema Sakaja kwa madai ya utepetevu kazini.
Madai hayo yanajumuisha kutolewa kwa huduma mbovu za matibabu hospitalini, miundombinu mibovu na utawala wa kaunti ya Nairobi kushindwa kukusanya taka kwa manufaa ya wakazi wa Nairobi.
Wakati wa mkutano wao na Raila, Sakaja na wawakilishi wadi hao walikubaliana kusuluhisha tofauti zao ndani ya mwezi mmoja.
Wakiwahutubia wanahabari jana Jumatatu, wawakilishi wadi wa kaunti ya Nairobi waliapa kuwasilisha hoja ya kumtimua Sakaja madarakani wakisema ameshindwa kuchapa kazi.
Wakiimba nyimbo za kudhirihisha azimio lao, wawakilishi hao walielezea imani kwamba watakusanya saini zaidi ya 100 kama ishara kwamba imani yao kwa Gavana huyo imefifia.
“Tumeamua kumpiga teke Sakaja, na kamwe hatutarudi nyuma,” waliimba MCAs hao wakati moshi wa kumfurusha Gavana huyo madarakani ukizidi kuifunika anga ya Nairobi.
“Tunasema kwamba ili Nairobi iwork tena, Sakaja must go! Ili barabara zijengwe, Sakaja must go!”
Kufuatia mkutano kati yao na Raila, shoka la kumbandua Sakaja madarakani huenda likapozwa kwa muda.