Kiongozi wa upinzani Raila Odinga ametishia kurejelea maandamano mwakani kama njia ya kushinikiza serikali kuondoa sheria mpya ya kifedha ya mwaka 2023.
Akizungumza nyumbani kwake huko Bondo alipohudhuria mashindano ya kuendesha mitumbwi, Raila alisema kwamba sheria hiyo ya kifedha imezidishia wakenya matatizo.
“Tunasema mwaka mpya mpaka hii sheria ya kodi itolewe, hiyo Finance Bill mpaka itolewe, wasipotoa hiyo sheria ya fedha tutarudi kwenye uwanja.” alisema Raila.
Aliendelea kulaumu serikali ya Kenya Kwanza kwa kile alichokitaja kuwa kutoa ahadi za uwongo wakati wa kampeni hasa ile ya kupunguza gharama ya maisha.
Ahadi hizo kulingana naye zilikuwa za kuhadaa wakenya kuwapigia kura na baada ya kuingia madarakani wamekosa kuzitimiza.
James Orengo ambaye ni gavana wa Siaya ambaye pia alihudhuria shindano hilo la kuendesha mitumbwi alisema anaamini iwapo Raila angekuwa Rais mambo yangekuwa tofauti.