Kiongozi wa upinzani Raila Odinga anapendekeza vyama vya kisiasa kupitia kwa kundi la wawakilishi wa vyama bungeni, IPPG vihusishwe katika mchakato wa kuwateua makamishna wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, IEBC.
Raila amedokeza kuwa IPPG yafaa ihusishwe katika uundaji wa IEBC sawa na ilivyokuwa mwaka 1997 kabla ya ya uchaguzi mkuu.
Haya yanajiri wakati ambapo kamati ya majadiliano yanayoendelea kati ya serikali na upinzani inatarajiwa kukutana Ijumaa wiki hii, ili kujumuisha maoni na mapendekezo kutoka kwa pande zote mbili.
Muungano wa upinzani umesema kuwa ni bora ikiwa vyama vya kisiasa vitawateua makamishna wa IEBC badala ya kubuni jopo kuteua wanachama wengine wa tume hiyo.
Upinzani pia unapendekeza kuondolewa kwa afisi iliyopo ya IEBC ikiongozwa na afisa mkuu mtendaji Marjan Hussein.
IEBC ililemazwa na kushindwa kutekeleza majukumu yake kikamilifu baada ya kuondolewa afisini kwa makamishna wanne pamoja na kustaafu kwa mwenyekiti wake Wafula Chebukati.