Kiongozi wa upinzani Raila Odinga amesisitiza kujitolea kwake kuhusu mazungumuzo kati ya serikali na upinzani, yatakahoandaliwa Jumatatu ijayo, lakini akaonya dhidi ya jaribio lolote la kunyamazisha upinzani.
Aidha Raila alisema Muungano wa Azimio la umoja, litashiriki mazungumuzo hayo mradi maswala yanayowahusu wakenya yanapewa kipa umbele.
Kwa mara nyingine Raila alisema kuwa muungano wa Azimio hauna nia ya kujiunga au kugawana mamlaka na serikali, akisema maswala wanataka yaangaziwe ni bayana.
Muungano huo wa Azimio la Umoja One Kenya, uliikosoa kanisa kwa kukosa kushtumu dhuluma za polisi zilizoripotiwa wakati wa maandamano ya hivi maajuzi dhidi ya serikali.
Muungano huo pinzani pia unalitaka kanisa kumkosoa Inspekta Jenerali wa polisi Japhet Koome kwa kudai kwamba upinzani ulikodisha miili kutetea maandamano yao dhidi ya serikali.
Kinara huyo wa upinzani alikuwa akiongea wakati wa ibada ya kanisa katika kaunti ya Kisumu.
Aidha aliitaka serikali kutambua na kuheshimu haki ya kikatiba ya Wakenya ya kuandamana.