Kiongozi wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya Raila Odinga amesema kwamba anakubaliana na vijana wa taifa hili kwamba haki inafaa kutekelezwa kabla ya mazungumzo kuandaliwa kutatua malalamishi yao.
Haya yanafuatia maandamano ya wiki kadhaa ya vijana wa Gen Z ambao wamekuwa wakishinikiza kuwepo kwa utawala bora nchini kuanzia kwa kuukataa mswada wa fedha wa mwaka 2024.
Raila sasa anasema kwamba anakubaliana na vijana hao kwamba kila mwathiriwa wa ukatili wa polisi wakati wa maandamano afidiwe na serikali, kesi za waliokamatwa kufuatia maandamano zitupiliwe mbali na wote waliokamatwa wakati wa maandamano waachiliwe huru.
Masuala mengine ambayo kiongozi huyo ameorodhesha ni pamoja na kutatuliwa kwa migogoro ya wafanyakazi wa sekta za afya na elimu haswa walimu wa JSS, kuondolewa kwa bima mpya ya Afya SHIF na kuendelezwa kwa NHIF pamoja na kushtakiwa na kuhukumiwa kwa maafisa wa usalama waliodhulumu watu waliokuwa wakiandamana kwa amani.
Kwenye taarifa ambayo ilipachikwa kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii, Raila anasema kwamba masuala hayo yatakaposhughulikiwa kikamilifu, basi anaweza kukubali mazungumzo ya kitaifa.
Anapendekeza kwamba vijana, viongozi serikalini, viongozi wa kidini, wataalamu wa sekta ya afya, mawakili na walimu wajumuishwe kwenye meza ya mazungumzo.
Masuala anayopendekeza yaangaziwe kwenye mazungumzo hayo ni utawala bora, gharama ya juu ya maisha, kukabiliana na ukabila na ufisadi na jinsi ya kushughulikia deni la taifa.
Taarifa ya Odinga inajiri wakati ambapo vijana wanaonekana kutoridhishwa na hatua yake ya kukubali kushiriki mazungumzo na serikali ya Kenya Kwanza huku vyama vingine vya muungano wa Azimio vikijitenga na mazungumzo hayo na nyadhifa za mawaziri.
Hata hivyo Odinga amekiri kwamba ameguswa na kujitolea kwa vijana wa taifa hili kupigania nchi yao.
Rais William Ruto alikuwa amependekeza kuunda serikali inayojumuisha wote ambapo muungano wa Azimio utapata nyadhifa za mawaziri na mazungumzo ya kitaifa ya sekta mbali mbali kushughulikia malalamishi ya vijana ambao wamekuwa wakiandamana.