Raia wa Lebanon leo Jumatano wameuhama mji wa kusini mwa nchi hiyo wa Tyre.
Hii ni baada ya jeshi la Israel kutoa maonyo kwa wakazi kuhama maeneo mengi ya mji huo ambao ni makazi ya maelfu ya watu waliopoteza makazi.
“Hali ni mbaya zaidi, tunawahamisha watu,” amesema Mortada Mhanna, ambaye ni mkuu wa kitengo cha usimamizi wa majanga cha mji wa Tyre.
Bilal Kashmar, afisa wa vyombo vya habari wa kitengo hicho, aliliambia shirika la habari la AFP kuwa watu wengi wanauhama mji huo na kuelekea katika maeneo ya viungani.
“Unaweza ukasema mji wote wa Tyre unahamwa,” alisema, akiongeza kuwa watu wengi tayari wameuhama mji huo ambao wakati mmoja ulikuwa na shughuli nyingi.
Watu tu wapatao 14,500 walikuwa bado mjini humo jana Jumanne, maelfu kati yao wakiwa waliopoteza makazi kutoka maeneo mengine ya kusini, aliiambia AFP.
Watu walianza kuhama punde baada ya jeshi la Israel kutoa wito kwa wakazi katika maeneo mengi ya mji wa Tyre kuondoka kabla ya kuanza kwa operesheni za kijeshi zinazolenga kundi la wanamgambo la Hezbollah nchini Lebanon.
September 23 mwaka huu, Israel ilianzisha mashambulizi makubwa ya anga nchini Lebanon, baada ya karibu mwaka mmoja wa mashambulizi ya kuvuka mpaka kati yake na kundi la Hezbollah juu ya vita katika eneo la Gaza.
Tangu wakati huo, watu wasiopungua 1,552 wameuawa katika mashambulizi ya Israel nchini Lebanon kulingana na takwimu zilizotangazwa na Wizara ya Afya na kujumulishwa na AFP.