Msako wa pamoja ulioratibiwa vizuri katika mtaa wa Mwaliko, mjini Mwea, umefichua mtandao unaoshukiwa kujihusisha na ulaghai wa mtandaoni unaoendeshwa na raia watatu wa Nigeria.
Watuhumiwa Peter Chukwujekwu, Alazor Chukulute Sunday na Nnalue Chiagozie Samwel, walinaswa baada ya raia wa kawaida kutoa taarifa kufuatia harakati za kutiliwa shaka na shughuli za usiku wa manane ndani ya nyumba yao ya kupangisha.
Wapelelezi walipopekua nyumba hiyo, walipata simu 21, kadi za SIM 79, kompyuta mpakato ya Dell na kadi nyingi za benki kutoka taasisi mbalimbali za kifedha, ishara ya mtandao wa ulaghai uliopangwa vizuri.
Uchunguzi umebaini kuwa watatu hao, ambao wanadai kuendesha biashara ya mtandaoni, wako nchini kinyume cha sheria, vibali vyao vya kuingia vikiwa vimekwisha muda na hawana vibali halali vya kufanya kazi.
Watatu hao kwa sasa wanazuiliwa rumande huku maafisa wa uchunguzi wakiendelea kufuatilia mtandao wao na kubaini uhusiano wowote na mitandao ya uhalifu wa kimtandao ya kuvuka mipaka.