Raia wa Ethiopia wanaozuru hapa nchini, sasa hawatalipa dola 30 ambazo wageni wanaoingia hapa nchini hulipa, kupitia mfumo wa kielektoniki ETA.
Balozi wa Ethiopia nchini Kenya Bacha Debele, alisema serikali ya Kenya haitawatoza raia wa nchi hiyo ada hiyo.
Katika ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa X Debele aliishukuru Kenya kwa kuchukua hatua hiyo, akisema ni afueni kwa raia wengi wa Ethiopia ambao awali walikabiliwa na changamoto kuingia humu nchini kutokana na vikwazo vya malipo.
“Naishukuru serikali ya Kenya kwa uamuzi wake wa busara wa kuwaondolea raia wa Ethiopia ada ya kuingia nchini Kenya,” alisema balozi Debele.
Debele aliwafahamisha raia wa Ethiopia kwamba, licha ya Kenya kuwaondolea malipo hayo, sharti la wao kujisajili kupitia mtandao, lingalipo.
“Tunawafahamisha raia wetu kwamba wanaweza ingia nchini Kenya bila hitaji la viza au malipo yoyote, lakini hitaji la kujisajili kupitia ETA kabla ya wao kuwasili Kenya lingalipo,” aliongeza balozi Debele.
Mnamo mwaka uliopita, Kenya iliondoa hitaji la viza kwa wageni wanaozuru taifa hili kutoka mataifa ya Bara Afrika.