Takriban wapiga kura milioni 44 watashiriki leo Alhamisi kwenye uchaguzi wa urais katika Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo DRC, ambao unawaniwa na wagombeaji 19.
Hata hivyo, hali ya kiusalama katika baadhi ya maeneo nchini humo pamoja na changamoto za uchukuzi zinatarajiwa kuathiri uchaguzi huo.
Jamhuri ya Congo ni taifa lenye utajiri mkubwa wa madini aina ya cobalt ambayo ni muhimu katika utengezaji wa betri za magari.
Endapo uchaguzi huo utaendeshwa ipasavyo,basi utachangia pakubwa katika kudumisha uthabiti nchini humo na kuhakikisha kwamba madini hayo yananufaisha raia wa nchini hiyo.
Rais Félix Tshisekedi ametoa wito kwa wapiga kura kumchagua tena kwa muhula wa pili.
Miongoni mwa wapinzani wake ni mfanyibiashara Moïse Katumbi na Martin Fayulu, ambaye anaamini kwamba yeye ndiye aliyeshinda uchaguzi wa urais wa mwaka 2018, ambao matokeo yake yalishukiwa na waangalizi wa kimataifa.