Mama wa Taifa Rachel Ruto ametoa wito wa uwekezaji wa haraka na ufadhili ili kusaidia shule, magereza na taasisi zingine za umma nchini kukoma kutumia kuni na badala yake kutumia nishati safi kwa upishi.
Akizungumza jijini Nairobi wakati wa kufungua mkutano wa siku mbili kuhusu uwekezaji wa upishi unaotumia nishati safi katika taasisi mbalimbali, Rachel alisema chakula katika taasisi nyingi nchini Kenya bado kinapikwa kwa kutumia kuni, jambo linalohatarisha afya za watu, mazingira na hali ya hewa.
Licha ya changamoto hizo, Mama Taifa alisema kuwa Kenya imepiga hatua.
Watu wanaotumia nishati safi kupika wameongezeka kutoka asilimia 10 mwaka 2013 hadi zaidi ya asilimia 30 mwaka 2023, ikiashiria mafanikio yanayoweza kuongezeka zaidi kupitia ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi.
Lakini barani Afrika kwa ujumla, hali bado ni mbaya kwani takribani familia nne kati ya tano bado hazina nishati safi za kupika, na ni asilimia 23 pekee ya watu wanaotumia teknolojia za kisasa.
Mama Taifa alisisitiza kuwa hali hii inaathiri zaidi wanawake na watoto.
Alithibitisha lengo la Kenya la kuhakikisha kila mtu anapata nishati safi za kupikia ifikapo mwaka 2028, akisema lengo hilo si sera tu, bali ni ahadi — kwamba hakuna mama wala mtoto atakayeteseka kwa gharama ya kupika kwa kuni.