R. Kelly na kampuni ya Universal kutoa pesa za kulipa wahanga wake

Marion Bosire
2 Min Read

Jaji wa mahakama ya wilaya ya mashariki ya New York nchini Marekani Ann Donnelly ameamuru kwamba mwanamuziki R. Kelly na kampuni ya muziki ya Universal lazima watoe dola nusu milioni ambazo zitatumika kufidia wahanga wake na kulipa faini mbali mbali za mahakama ambazo hajalipa.

Donnelly alitoa agizo hilo Jumatano Agosti 23, 2023, akisema kampuni ya muziki ya Universal inashikilia dola 567,444.19 ambazo zilitokana na mirahaba ya muziki wake na lazima zitolewe ili kutumika kwa sababu alizozitaja.

Zitakapotolewa, fedha hizo zitatumwa kwa waendesha mashtaka wa Brooklyn ambao watazigawa kwa wahanga wa mwimbaji huyo.

Kelly kwa sasa anahudumia kifungo chake cha miaka 30 gerezani tangu mwaka jana na alijipata pabaya baada ya kushtakiwa na watu ambao aliwahi kudhulumu kingono wengi wao wakiwa chini ya umri wa utu uzima kulingana na sheria za Marekani.

Alipohukumiwa kifungo hicho mwaka 2021, kampuni za muziki za Universal na Sony ziliagizwa kutoa dola laki 5 kugharamia kesi za Kelly na fidia kwa waathiriwa kwani mahakama ilikuwa na imani kwamba zilikuwa zinashikilia pesa za mwimbaji huyo.

Kulingana na uamuzi wa hivi punde wa mahakama kampuni ya Sony haitalazimika kutoa pesa zozote na sasa Universal ndiyo itatoa pesa hizo zote.

Tetesi za Kelly kudhulumu watoto kingono zilisheheni tangu miaka ya 90 lakini uchunguzi uliosababisha kukamatwa kwake na kushtakiwa ulijiri baada ya harakati za mtandaoni almaarufu “#MeToo” na filamu ya matukio halisi kwa jina “Surviving R. Kelly” ambayo ilizua ghadhabu ulimwenguni kote.

Alipatina na hatia kwenye makosa 9 ya kingono, matatu yanayohusisha watoto ambao aliwalazimisha kushiriki ngono na matatu ya kuandaa video za ngono zinazohusisha watoto.

Share This Article