Qatar imetangaza kusitishwa kwa juhudi za kupatanisha Israel na Hamas hadi pale ambapo pande husika zitadhihirisha utayari na umakini wa kusitisha vita.
Haya yanajiri baada ya wanajeshi wa Israeli kuua watu wapatao 32 katika shambulizi la usiku katika eneo la Jablia kaskazini mwa Gaza, kulingana na wanahabari.
Shambulizi hilo linajiri siku moja tu baada ya Israel kuua wapalestina 44 katika eneo la Gaza na watu 31 huko Lebanon.
Utathmini wa umoja wa mataifa unaonya pia kwamba huenda baa la njaa likakumba maeneo ya Gaza kaskazini huku vita vikichacha na misaada kuzuiwa kuingia humo.
Mashambulizi ya Israel katika eneo la Gaza yamesababisha vifo vya wapalestina 43,552 huku wengine 102,765 wakijeruhiwa tangu vita vilipozuka Oktoba 7, 2023.
Watu wapatao 1,139 waliuawa nchini Israel katika mashambulizi yaliyoongozwa na Hamas siku hiyo huku wengine zaidi ya 200 wakichukuliwa kama mateka.
Huko Lebanon wati 3,136 wameuawa na wengine 13,979 kujeruhiwa tangu Israel kuanza kushambulia nchi hiyo.