Profesa Abraham Kithure Kindiki ataapishwa leo katika ukumbi wa KICC kuwa Naibu Rais katika hafla ambayo itang’oa nanga rasmi saa nne asubuhi.
Prof. Kindiki tayari amemkabidhi mikoba Musalia Mudavadi ambaye atahudumu kama kaimu Waziri wa Usalama wa Kitaifa.
Wadhifa huo ulishikiliwa na Pof. Kindiki kabla ya kuteuliwa kuwa Naibu Rais.
Kindiki atakuwa Naibu Rais wa 14 tangu Kenya ijinyakulie uhuru mwaka 1963 na Naibu Rais wa tatu tangu kuidhishwa kwa katiba mpya ya mwaka 2010.
Hafla hiyo ya Ijumaa ambayo imetangazwa kuwa sikukuu inahudhuriwa na maelfu ya Wakenya waliofika kutoka matabaka mbalimbali, viongozi na pia mabalozi wanaowakilisha mataifa yao humu nchini.
Pia afisi ya Naibu Rais itakuwa afisi kubwa zaidi kwa Prof. Kindiki aliye na umri wa miaka 52 baada ya kuhudumu kama Seneta wa Tharaka Nithi kati ya mwaka 2013 hadi 2022.
Prof. Kindiki aliteuliwa Waziri wa Usalama wa Kitaifa mwaka 2022 baada ya uchaguzi mkuu kumrithi Dkt. Fred Matiang’i.
Awali, Prof. Kindiki alimwakilisha Rais William Ruto kama wakili wake kwenye ya mahakama ya ICC.