Mwana wa mfalme Harry ameshindwa kwenye kesi ambapo alikuwa ameishtaki serikali ya Uingereza katika mahakama kuu kuhusu ulinzi wake akiwa nchini Uingereza.
Harry aliamua kutumia mahakama kupinga hatua ya kupunguza ulinzi wake punde alipokoma kuwa mwana mfalme anayehudumu kwenye ufalme.
Aliambia mahakama kwamba alihisi kwamba haki zake zimehujumiwa kwa mabadiliko yaliyofanywa kwa ulinzi wake kutoka kwa maafisa wa polisi ikitizamiwa kwamba bado anakumbana na hatari za kiusalama.
Sasa anasema atakata rufaa kutafuta kubatilisha uamuzi wa mahakama unaosema kwamba hakuna sheria ilikiukwa kwa kumpunguzia ulinzi.
Mawakili wake wanasema kwamba Harry hatafuti kupendelewa lakini kumekuwa na ukiukaji wa haki zake za msingi hasa hatua ya kupunguza ulinzi kutoka kwa polisi wanaolipwa na ushuru wa wananchi.
Alipoamua kuacha kuwa kwenye familia ya ufalme nchini Uingereza na kuhamia nchini Marekani, Harry alikoma kupokea ulinzi sawa na aliokuwa akipata awali kutoka kwa polisi.
Badala yake ulinzi wake huamuliwa kila mara anapozuru Uingereza sawa na wanavyofanyiwa wageni wa hadhi ya juu wanaozuru Uingereza.
Mahakama kuu nchini Uingereza inashikilia kwamba kamati inayoshughulikia masuala ya ulinzi wa watu wa familia ya kifalme na wageni wengine mashuhuri kwa jina “Ravec” ilichukua hatua faafu.