Polisi wasambaratisha biashara haramu ya unga Nairobi

Kupitia ukurasa wa X, DCI ilisema washukiwa saba walikamatwa wakiendesha biashara hiyo haramu na wanazuiliwa huku uchunguzi ukiendelea.

Tom Mathinji
2 Min Read
Makao Makuu ya Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI).

Maafisa wa polisi wametibua biashara haramu ya uuzaji wa unga, katika kaunti ndogo ya Kasarani, kaunti ya Nairobi.

Maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), walitekeleza msako kwenye ghala moja katika eneo la Canaan, Kasarani na kupata shughuli za upakiaji upya wa unga kwa kutumia mifuko bandia.

Kupitia ukurasa wa X, DCI ilisema washukiwa saba walikamatwa wakiendesha biashara hiyo haramu na wanazuiliwa huku uchunguzi ukiendelea.

“Uchunguzi umebainisha kuwa ghala hilo limebadilishwa na kuwa kituo cha upakiaji haramu wa unga na kisha kusambazwa baada ya kuwekwa nembo bandia, hatua inayowahadaa wateja,” ilisema DCI kwenye ukurasa huo wa X.

Waliokamatwa ni pamoja na Felix Kiprop, ambaye ni mfanyakazi wa kampuni ya Unga ya SARA, Cynthia Nakoli, afisa wa mauzo kutoka kampuni hiyo, wapakiaji mizigo Joseph Kariuki na Victor Omondi Opiyo, dereva Daniel Ngugi, wakiwemo Maria Ngui na Samuel Kimilu, ambao walipatikana katika eneo la mkasa.

Maafisa hao walinasa mifuko 3,682 ya unga wa mahindi yenye thamani ya shilingi 312,120, lori aina ya Hyundai lenye nambari za usajili KBR 092K, vifaa vya viwanda, mashini za kupima uzani pampoja na vifaa vya kuweka tarehe na nembo za kampuni.

“DCI imeelezea kujitolea kwake kukabiliana na biashara ya bidhaa haramu na kuwalinda watumiaji bidhaa wa Kenya dhidi ya bidhaa hatari kwa matumizi ya binadamu.

TAGGED:
Share This Article