Maafisa wa idara ya upelelezi wa makosa ya jinai DCI wamempiga risasi jambazi aliyekuwa sehemu ya genge ambalo huwahangaisha wakazi katika soko la Ogembo, kaunti ya Kisii.
Maafisa hao walipata habari kwamba majambazi watatu waliokuwa wamejihami, walipanga kutekeleza wizi katika duka moja la Mpesa katika eneo hilo.
Maafisa hao walijiandaa kukabiliana na wahalifu hao, lakini majambazi hao waliwatambua maafisa hao mapema na kuwafyetulia risasi.
“Maafisa wa polisi walikabiliana na majambazi hao na kumjeruhi mmoja wao vibaya. Wezake wawili walitorokea katika mto ulio karibu,” ilisema idara ya DCI kupitia mtandao wa X.
Baada ya kumpekua jamabazi aliyepigwa risasi, maafisa hao walipata bastola iliyokuwa na risasi moja.
“Juhudi za kuwatafuta majambazi waliotoroka zinaendelea,” ilisema idara hiyo huku ikitoa wito kwa wananchi kuripoti kuhusu visa vyovyote vya kutiliwa shaka.