Polisi waimarisha ulinzi na ukaguzi wa trafiki msimu huu wa Pasaka

Maafisa wa ziada wametumwa kuimarisha doria na uangalizi katika maeneo ya umma.

Marion Bosire
2 Min Read

Huduma ya Taifa ya Polisi, NPS imetangaza kuimarishwa kwa hatua za usalama na utekelezaji wa sheria za trafiki nchi inapojiandaa kwa likizo ya Pasaka.

Sikukuu ya Pasaka imesadifiana pia na kufungwa kwa shule kwa likizo ya mwezi wa nne baada ya kukamilika kwa muhula wa kwanza wa mwaka huu wakati ambapo mvua kubwa pia inashuhudiwa nchini.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari leo, NPS ilihakikishia Wakenya, wakazi na wageni usalama wao katika kipindi kinachotarajiwa kushuhudia ongezeko la safari, mikusanyiko ya kijamii na shughuli za utalii.

Huduma hiyo ilibainisha kuwa mambo haya yanawasilisha changamoto za kipekee za usalama zinazohitaji juhudi za pamoja.

Ili kukabiliana na hali hiyo, NPS kwa kushirikiana na mashirika mengine ya serikali, imeongeza operesheni kote nchini kuhakikisha uzingatiaji wa usalama barabarani.

Watumiaji wa barabara hata wanaotembea kwa miguu, waendesha boda boda na waendeshaji wa magari ya uchukuzi wa umma wamehimizwa kuwa waangalifu na kufuata kikamilifu sheria za trafiki.

Hatua muhimu za usalama zilizosisitizwa ni pamoja na kuzingatia viwango vya mwendo, kuvaa vifaa vya kujikinga, kuepuka kupakia kupita kiasi na kujiepusha na kuendesha magari wakiwa walevi au wakitumia simu.

Madereva pia wameshauriwa kuhakikisha magari yao yako katika hali bora kupitia matengenezo ya mara kwa mara ili kupunguza ajali zinazotokana na hitilafu za kiufundi.

Aidha, NPS katika taarifa iliyotiwa saini na msemaji wake Muchiri Nyaga, imebainisha kwamba maafisa wa ziada wametumwa kuimarisha doria na uangalizi katika maeneo ya umma kama maduka makubwa, maeneo ya ibada, masoko na vituo vya usafiri.

Huduma hiyo imewataka wananchi kubaki macho na kuripoti shughuli zozote za kutiliwa shaka kupitia njia rasmi za dharura, ikithibitisha dhamira yake ya kulinda maisha na mali.

Share This Article