Maafisa watano wa polisi wa Kenya walikamatwa na polisi wa Tanzania na kuzuiliwa kwa muda katika eneo la Rombo nchini Tanzania baada ya kuvuka mpaka na kuingia kwenye himaya ya taifa hilo jirani.
Hatua hiyo ya polisi wa Tanzania ilifuatia wito uliotolewa na raia mmoja wa Tanzania ambaye alikuwa amekamatwa na polisi wa Kenya katika eneo la Tarakea kwa kushukiwa kuhusika na wizi wa magari nchini Kenya.
Polisi hao watano wa kituo cha polisi cha Buruburu jijini Nairobi walikuwa wanafuatilia washukiwa wa njama ya wizi wa magari kutoka Kenya hadi Tanzania walipokamatwa Ijumaa alasiri.
Walikuwa wamekamata mshukiwa mmoja raia wa Kenya ambaye alikuwa anawaelekeza kwa mshukiwa mwenzake kwa kutumia barabara zisizo rasmi na wakajipata nchini Tanzania.
Maafisa hao wa Kenya walitafuta usaidizi kutoka makao makuu ya polisi jijini Nairobi na wenzao wa eneo la Kajiado Kusini wakatumwa kuwaokoa.
Naibu Kamishna wa kaunti Anthony Macharia aliongoza kundi kutoka Kenya ambalo lilifanya mazungumzo na polisi wa Tanzania na mwafaka ukaafikiwa na kusababisha kuachiliwa kwa maafisa hao watano wa usalama wa Kenya.
Mshukiwa huyo raia wa tanzania hata hivyo hakupeanwa kwao.