Timu ya Police FC imefanya mazoezi ya mwisho mapema Jumamosi uwanjani Abebe Bikila nchini Ethiopia, kujiandaa kwa marudio ya mchujo wa kwanza wa mechi ya kombe la Shirikisho dhidi ya wenyeji Ethiopian Coffee SC siku ya Jumapili.
Waakilishi wa Kenya,Police watahitaji sare ya magoli katika mechi ya kesho alasiri ili kufuzu kwa mchujo wa pili na wa mwisho baada ya kuambulia sare tasa wiki iliyopita katika uwanja wa Nyayo.
Mshindi wa mchuano wa Jumapili ataweka miadi ya kuchuana na mabingwa watetezi Zamalek ya Misri katika mchujo wa pili.
Ni mara ya kwanza kwa Police kushiriki mashindano ya Afrika tangu wapandishwe ngazi kucheza Ligi Kuu Kenya.