Police FC kupanda mchongoma Cairo Ijumaa

Dismas Otuke
1 Min Read

Police FC ya Kenya itakuwa na kibarua cha mwaka leo Ijumaa usiku jijini Cairo itakapokabiliana na mabingwa watetezi Zamalek ya Misri katika marudio ya mchujo wa pili kuwania kombe la Shirikisho Afrika.

Police waliopoteza bao moja bila jibu Jumamosi iliyopita katika uwanja wa kitaifa wa Nyayo, wanahitaji ushindi wa mabao mawili kwa bila dhidi ya wenyeji leo ili kufuzu kwa hatua ya makundi ya kombe hilo.

Wanashiriki kipute hicho kwa mara ya kwanza baada ya kutwaa kombe la FKF msimu jana na walitinga mchujo wa pili baada ya kuwatema Ethiopia Bunna bao moja kwa nunge.

Kwa upande wao, Zamalek ambao pia ni washindi mara 14 wa Ligi Kuu nchini Misri na washindi mara tano wa Ligi ya Mabingwa Afrika, walifuzu kwa raundi ya pili bila kucheza mechi baada ya kutwaa kombe hilo msimu uliopita walipoibwaga RS Berkane ya Morocco.

Mechi hiyo itang’oa nanga saa mbili juu ya alama Ijumaa usiku.

Website |  + posts
Share This Article