Ndoto ya Kenya Pipeline kufuzu kwa fainali ya Kombe la kilabu bingwa Afrika kwa akina dada kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2023, ilizimwa jana baada ya kuzidiwa maarifa na mabingwa watetezi Zamalek ya Misri , seti 3-2, kwenye nusu fainali mjini Abuja, Nigeria.
Pipeline walishindwa kwa alama za 23-25, katika seti ya kwanza kabla ya kutwaa seti ya pili 28-26, lakini wakapoteza seti ya tatu 19-25.
Vipusa hao wa humu nchini walijikaza kisabuni na kushinda seti ya 4 alama 26-24, na kulazimu seti ya mwisho ya tano ichezwe kuwatenganisha.
Zamalek walinyakua seti hiyo alama 15-12, na kuweka miadi ya kumenyana na mahasimu wa nyumbani Al Ahly, katika fainali ya Jumapili .
Ahly walifuzu kwa fainali baada ya kuicharaza Carthage kutoka Tunisia, seti 3-0 za 25-15, 25-23 na 25-21.
Pipeline ndiyo timu pekee ya Kenya iliyofika hatua ya nusu fainali kati ya waakilishi watatu .
Mabingwa mara tano wa Afrika,Pipeline watapambana na Carthage ya Tunisia, kuwania nafasi ya tatu na nne kesho kabla ya fainali.