Peetah Morgan wa Morgan Heritage afariki

Marion Bosire
1 Min Read

Peter Anthony Morgan, mwimbaji mkuu katika bendi ya Morgan Heritage kutoka Jamaica amefariki akiwa na umri wa miaka 46. Kulingana na ujumbe kutoka kwa familia hiyo, Peetar Morgan aliaga dunia Jumapili Februari 25, 2024.

Wanachama wa bendi hiyo ya Morgan Heritage, ambayo imewahi kushinda tuzo ya Grammy, ni watoto wa mwimbaji Denroy Morgan.

Familia ya Morgan ilitoa taarifa hiyo kupitia kwa akaunti za mitandao ya kijamii za bendi yao ila haikuelezea kwa undani kilichosababisha kifo cha Peetar.

Kwenye taarifa hiyo marehemu alirejelewa kama mume, baba, mwana na ndugu.

Bendi ya Morgan Heritage ilianzishwa mwaka 1994 na kazi zao ni pamoja na albamu kwa jina “Protect Us Jah” ya mwaka 1997 na nyingine “Don’t Haffi Dread” ya mwaka 1999.

Iliibuka mshindi katika kitengo cha albamu bora ya mtindo wa reggae kwenye tuzo za Grammy za mwaka 2015, kupitia kwa albamu “Strictly Roots”.

Miaka miwili baadaye waliwasilisha albamu iitwayo “Avrakedabra” kwa ajili ya tuzo hiyo hiyo lakini wakashindwa na albamu ya “Stony Hill” yake Damian Marley mwanawe Bob Marley.

Share This Article