Paul Biya kupata Naibu Rais kwa mara ya kwanza kabisa

Bunge lilipitisha mswada wa kurejesha wadhifa wa Naibu Rais Jumamosi.

Marion Bosire
2 Min Read

Rais wa Cameroon Paul Biya sasa atapata Naibu Rais kwa mara ya kwanza kabisa katika uongozi wake uliodumu yapata miongo minne sasa.

Hii ni baada ya mabadiliko ya kikatiba yaliyojaa utata kutekelezwa nchini humo na kupata uungwaji mkono kutoka kwa bunge la nchi hiyo.

Wadhifa wa Naibu wa Rais uliondolewa nchini Cameroon mwaka 1972.

Ina maana kwamba sasa, iwapo chochote kitamtokea Biya wa umri wa miaka 93, ambaye ndiye kiongozi wa nchi mkongwe kabisa ulimwenguni, hakutakuwa na ombwe katika uongozi wa nchi hiyo kwani Naibu Rais atachukua uongozi mara moja na kukamilisha muhula.

Awali, sheria ya Cameroon ilielekeza kwamba iwapo chochote kingemsibu Rais na kumzuia kutekeleza majukumu yake, kiongozi wa bunge la Seneti angechukua uongozi kama kaimu Rais hadi uchaguzi uandaliwe.

Mchakato wa kurejesha wadhifa wa Naibu Rais hata hivyo umetiliwa shaka na viongozi wa upinzani wanaosema kwamba ulitekelezwa haraka bila umakini na unalenga kuweka mamlaka makuu katika wadhifa mmoja.

Haya yanajiri wakati ambapo hali ya kiafya ya Biya imekuwa ikitiliwa shaka.

Bunge la Cameroon liliandaa kikao cha pamoja Jumamosi na kupitisha mswada wa mabadiliko hayo na sasa unasubiri tu saini ya Rais ili uwe sheria.

Wabunge 200 walinga mkono mswada huo, 18 wakaupinga huku wanne wakikosa kuupigia kura.

Share This Article