Mwanamuziki wa Congo Papa Noel Nedule ameaga dunia. Anaaminika kukata roho akiwa jijini Brussels nchini Ubelgiji.
Papa Noel anafahamika sana kwa albamu yake iitwayo “Bel Ami” aliyozindua mwaka 2000 kando na kuhusika katika bendi mbali mbali kama mpiga gitaa.
Jina lake halisi ni Antoine Nedule Monswet na alizaliwa Disemba 25, 1940 siku ya krismasi ndiposa akabandikwa “Noel”.
Aliwahi kuwa mwanachama wa bendi ya mtindo wa soukous ya TPOK Jazz, iliyokuwa ikiongozwa na François Luambo Makiadi, na ambayo ilitawala tasnia ya muziki nchini Congo miaka ya 1950 hadi 1980.
Alikuwa mwanachama mwanzilishi wa bendi ya Kekele iliyoanzishwa mwaka 2000 na alihudumu pia kama kiongozi wake.
Hata hivyo matatizo ya kiafya yalimfanya akose kuhudhuria hafla muhimu za bendi kama vile matamasha na hata hafla za kurekodi nyimbo.