Naibu Mkuu wa Wafanyakazi katika Idara ya Utendakazi na Usimamizi katika Ofisi ya Rais Eliud Owalo ndiye atakayeongoza kamati ya kitaifa maandalizi ya mazishi ya aliyekuwa mchezaji nyota wa timu ya taifa Harambee Stars.
Naibu mwenyekiti wa kamati hiyo atakuwa Katibu wa Michezo Peter Tum.
Familia ya marehemu imetangaza hayo kupitia taarifa iliyotiwa saini na kakake Antony Origi.
Owalo alikuwa rafiki wa kufa kuzikana wa mwenda zake ambaye pia alifahamika kama “Makamu.”
Wanachama wengine wa timu hiyo ni mwenyekiti wa timu ya Gor Mahia Ambrose Rachier, mwenyekiti wa timu ya AFC Leopards Dan Shikanda, mwenyekiti wa timu ya Shabana FC Jared Nevton na yule wa timu ya Kakamega Homeboys FC Cleopa Shimanyula.
Mkuu wa kitengo cha michezo cha shirika la utangazaji nchini, KBC Elynah Shiveka pia amejumuishwa kwenye kamati hiyo.
Marehemu Austin Oduor amepangiwa kuzikwa Novemba 9, 2024 nyumbani kwake katika kijiji cha Makunga, kaunti ya Kakamega.
Oduor alilelewa mtaani Ziwani, Nairobi na alianza kupiga soka mwaka 1976 katika klabu ya Umeme FC, wakati huo akiwa mwanafunzi wa Highway Secondary kabla ya kujiunga na Gor Mahia mwaka 1980.
“Makamu” alikuwa Naibu Kapteni wa Gor Mahia ilipotwaa ubingwa wa Ligi Kuu mwaka 1983 na 85, na ni mwaka 1985 alipoitwa kwenye timu ya taifa kwa mara ya kwanza.
Hata hivyo, alisubiri hadi mwaka 1987 kabla ya kuanza kupata nafasi za mara kwa mara kuichezea Kenya, na anakumbukwa kwa mchango mkubwa ambapo kwa mara ya kwanza Harambee Stars ilifuzu kwa fainali za AFCON mara tatu mtawalia.
Mwaka 1990, Oduor alikuwa kocha na mchezaji wa Gor kufuatia kujiuzulu kwa kocha mkuu, lakini aliteuliwa kocha rasmi mwaka 1994 na 1996.