Owalo amwomboleza Austin Oduor

Dismas Otuke
2 Min Read

Naibu Msimamizi wa Ikulu Eliud Owalo ametuma risala za rambirambi kufuatia kifo cha mchezaji nyota wa zamani wa timu ya taifa Harambee Stars na nahodha wa Gor Mahia Austin  ‘Makamu’ Origi  Oduor aiyefariki jana Jumanne.

Oduor alikuwa kakake mshambulizi wa zamani wa Harambee Stars Mike Okoth na babake mlinda lango wa zamani wa Kenya Arnold Origi.

Oduor aliyecheza katika safu za kiungo na ulinzi pia ni mjombake  mshambulizi wa zamani wa Liverpool, AC Milan na timu ya taifa ya Ubelgiji Divock Origi.

Owalo amemtaja Origi kuwa mmoja wa wachezaji bora sana wa Kenya na pia rafiki wake wa karibu.

Oduor alilelewa mtaani Ziwani, Nairobi na alianza kupiga soka mwaka 1976 katika klabu ya Umeme FC, wakati huo akiwa mwanafunzi wa Highway Secondary kabla ya kujiunga na Gor Mahia mwaka 1980.

“Makamu” alikuwa Naibu Kapteni wa Gor Mahia ilipotwaa ubingwa wa Ligi Kuu mwaka 1983 na 85,na ni mwaka 1985 alipoitwa kwenye timu ya taifa kwa mara ya kwanza.

Hata hivyo, alisubiri hadi mwaka 1987 kabla ya kuanza kupata nafasi za mara kwa mara kuichezea Kenya, na anakumbukwa kwa mchango mkubwa ambapo kwa mara ya kwanza Harambee Stars ilifuzu kwa fainali za AFCON mara tatu mtawalia.

Mwaka 1990, Oduor alikuwa kocha na mchezaji wa Gor kufuatia kujiuzulu kwa kocha mkuu, lakini aliteuliwa kocha rasmi mwaka 1994 na 1996.

Share This Article