Aliyekuwa Gavana wa kaunti ya Kakamega Wycliffe Oparanya ametangaza kumuunga mkono Seneta wa sasa wa kaunti hiyo Dkt. Boni Khalwale kuwania wadhifa wa ugavana wa kaunti hiyo wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
Dkt. Khalwale alijaribu kumbandua Oparanya kutoka wadhifa huo wakati wa uchaguzi wa mwaka 2017 lakini akalambishwa sakafu.
“Katika siasa hakuna maadui wa kudumu, kilichopo ni kupigania maslahi,” alisema Oparanya nyumbani kwake huko Butere wakati akimuidhinisha Dkt. Khalwale kuwania wadhifa huo. Awali, wawili hao walikuwa mahasimu wa kupindukia kisiasa.
Mbunge wa Lurambi Titus Khamala na aliyekuwa mbunge wa Shinyalu Justus Kizito ni miongoni mwa wanasiasa wa eneo hilo waliokuwepo wakati wa hafla hiyo.
Dkt. Khalwale anasema miezi miwili iliyopita, alimtembelea Rais William Ruto na kumjuza kuwa atawania wadhifa wa ugavana wa kaunti ya Kakamega ifikapo mwaka 2027.
Rais Ruto alitekeleza wajibu muhimu katika kuwapatanisha Dkt. Khalwale na aliyekuwa Seneta wa kaunti ya Kakamega Cleophas Malalah wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2022.
Chini ya mapatano hayo, ilikubaliwa kuwa Malalah awanie wadhifa wa Ugavana wakati Dkt. Khalwale akiwania Useneta.
Huku Dkt. Khalwale akiibuka mshindi wa wadhifa huo, Malalah naye alibwagwa na Gavana wa sasa wa kaunti ya Kakamega Fernandes Barasa anayesemekana kukwaruzana na Oparanya kisiasa.
Barasa aliyechaguliwa kwenye wadhifa huo kwa tiketi ya chama chama ODM aliungwa mkono na Oparanya wakati huo.
Hatua ya Oparanya kumuunga mkono Dkt. Khalwale huenda ikazua siutofahamu ya kisiasa katika kaunti ya Kakamega kwani Oparanya ni mwandani wa kiongozi wa ODM Raila Odinga.
Kumekuwa na ripoti kwamba ODM huenda ikamuunga mkono mwakilishi wa wanawake wa kaunti ya Kakamega Elsie Muhanda kuwandia ugavana ifikapo mwaka 2027.
Dkt. Khalwale ni mwanachama wa chama kinachotawala cha UDA ambacho kiongozi wake ni Rais Ruto, chama ambacho Malalah ni katibu wake mkuu.
Malalah amekuwa akionyesha dalili za kuwania tena wadhifa wa ugavana wa Kakamega ifikapo 2027.