Mchekeshaji Eric Omondi anapanga kuandaa mnada leo Jumatatu Juni 3, 2023 kuuza viatu vyake ili kufadhili mwanamuziki Stevo Simple Boy ambaye ametumbukia kwenye lindi la umaskini.
Akizungumza kwenye mahojiano, mchekeshaji huyo alisema atauza jozi tatu za viatu vyake vinavyofahamika sana mitandaoni na pesa zote atakazopata zitamwendea Simple Boy.
Omondi alionekana akiwa amevaa viatu vikubwa vya rangi nyeupe wiki jana akielekea nchini Tanzania kwa tamasha, na ni mojawapo ya jozi atakazonadi hii leo.
Haya yanajiri baada ya mchekeshaji huyo kumtembelea Simple Boy nyumbani kwake ambapo alimpelekea mchango wa chakula.
Hata hivyo, alikashifiwa na Oga Obina kwa kile Obina alikitaja kuwa mchango wa kiwango cha chini na ambao hautamsaidia Simple Boy kama msanii. Kulingana na Obina, Omondi alimpa Stevo pakiti moja ya sukari na chache za unga wa mahindi na anahisi sio mchango tosha. Alihisi Omondi alikuwa anatumia matatizo ya Simple Boy kujiendeleza mitandaoni.
Obina alisema kwamba Omondi alistahili kumpa Stevo Simple Boy kazi badala ya mchango huo ambao alikisia haukuzidi shilingi 2,000. Obina baadaye alionekana akimtafuta Simple Boy ili ampe kazi lakini baadaye ikabainika alikuwa tu anataka kumhoji.
Stevo Simple Boy alikosana na usimamizi wake ambao alidai kwamba haukuwa ukiwajibika na sasa amesalia maskini. Usimamizi huo ulikatiza mkataba kati yao na sasa mwanamuziki huyo anasema atajisimamia.
Wengi wamejitokeza kumsaidia akiwemo mbunge wa Mumias Mashariki Peter Salasya ambaye ameahidi kumpa makazi.