Ombi la wakimbizi wa ndani kwa ndani kwa serikali

Marion Bosire
2 Min Read

Wakimbizi wa ndani kwa ndani kutoka Nyandarua ambao wamekita kambi katika kijiji cha Kianjogu, wadi ya Salama katika kaunti ya Laikipia wameipa serikali makataa ya siku 21 iwapatie makao la sivyo wataandamana hadi ikulu.

Watu hao ambao wengi walikosa kufikiwa na mipango ya awali ya serikali ya kugawa ardhi, wanashangaa ni kwa nini serikali inachelewesha mpango wa kuwapa ardhi na fedha za kujijenga tena kama ilivyoahidi.

Mwaka 2017, serikali iliwapa watu hao elfu 50 kila mmoja na kuahidi kuwapa salio la elfu 150 kila mmoja mwaka jana ahadi ambayo haijatimizwa hadi sasa.

Kambi ya Jericho wanakoishi, ina watu 3600, wengi wao wakiwa kina mama wazee na watoto. Makazi yao ni ya makaratasi na hawana mahitaji muhimu kama vyoo na maji safi. Eneo hilo limejaa wanyama kama nyoka, tembo na fisi.

Mwonekano wa kambi ya Jericho

Mratibu wa kundi zima la wakimbizi James Mwaura, amesema kwamba wanashuku mateso yao yanasababishwa na watu fulani wenye ushawishi mkubwa.

Kulingana naye, watu hao wanataka kulemaza mpango wa kuwapa wakimbizi hao makazi mapya na kuishia kugawana ardhi hiyo wenyewe.

Kwa sasa wengi kati ya wakimbizi hao wanafanya kazi za vibarua katika vijiji vilivyo karibu, ambapo wanalipwa nwa vyakula na wala sio pesa.

Ripoti yake Lydia Mwangi.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *