Ombi la Mo Dewji la kufunga viwanda lakataliwa Tanzania

Marion Bosire
2 Min Read
Waziri Hussein Bashe

Serikali ya Tanzania kupitia kwa waziri wa Kilimo Hussein Bashe imekataa ombi la mwanabiashara Mohammed “Mo” Gulamabbas Dewji la kufunga kiwanda cha kutayarisha chai pamoja na vingine anavyomiliki.

Akizungumza jijini Dodoma jana, wakati wa kufungua kongamano kuhusu zao la chai, Bashe alielezea kwamba hatua yao ya kukatalia mbali ombi la Mo imechochewa na hitaji la kuepusha athari kama vile watu kupoteza nafasi za ajira.

Waziri huyo alisema kwamba iwapo wawekezaji wanakumbwa na changamoto yuko tayari kujadiliana nao ili kuzitatua na shughuli za viwanda hivyo ziendelee kama kawaida.

“Nimepokea barua ya kampuni ya Mohamed Enterprise kutaka kufunga Viwanda nimewaambia hawawezi kufunga viwanda, tujadiliane njia nyingine lakini sio kufunga kwa sababu kwetu bado sekta ya chai ni muhimu kwa ajira za Watu.” alisema waziri Bashe.

Alielezea pia kwamba Mo Dewji aliomba pia serikali ichukue mashamba yake na kuyaendeleza ambapo alisema kundi maalumu litabuniwa kwa ajili ya kukagua mali hiyo kwa ajili ya ubadilishanaji.

Bashe alihakikishia wananchi wa Tanzania kwamba serikali itatafuta namna ya kusuluhisha changamoto zilizopo na kuhakikisha sekta ya chai inaendelea ipasavyo.

Suala jingine alilozungumzia waziri Bashe ni kutathminiwa kwa viwango vya matozo ambapo alisema wanajadiliana na wizara ya fedha kuhusu hilo.

“Nimeongea na Waziri wa Uwekezaji ili hivi viwanda vipate nafuu ya kodi ya kuagiza nje kwasababu kama tunampa mtu wa export sehemu nafuu ya kodi, ukitazama sekta ya chai kwa ujumla bidhaa zake zinahusisha kusafirisha nje” alisema Bashe.

Mo Dewji anaendesha biashara nyingi za kiviwanda nchini Tanzania ambazo zilianzishwa na babake mzazi miaka ya 1970.

Yeye ndiye mfadhili mkuu wa timu ya soka ya Simba Sc nchini Tanzania.

Share This Article