Ombi la Diddy lakataliwa na jaji akisubiri hukumu Ijumaa

Marion Bosire
1 Min Read
P Diddy

Jaji ambaye anasikiliza kesi inayomkabili mwanamuziki wa Marekani Sean “Diddy” Combs’ jana Jumanne alikataa ombi la mwanamuziki huyo la kuondolewa hatia zinazohusu ukahaba.

Jaji Arun Subramanian, aliyesikiliza kesi hiyo kwa majuma manane huko New York alikataa kutupilia mbali hatia ya usafirishaji wa watu kwa ajili ya kuwatumia kingono ambayo hukumu yake ya juu kabisa ni miaka 10 gerezani.

Combs mwasisi wa kampuni ya muziki ya Bad Boy Records, anatarajiwa kuhukumiwa Ijumaa, Oktoba 3, 2025 na viongozi wa mashtaka wanata ahukumiwe kifungo cha miaka 11 gerezani huku mawakili wake wakitaka afungwe miezi 14 pekee.

Waongoza mashtaka hao wanamlaumu Combs kwa kuendesha shughuli hizo za ukahaba ambazo ni kinyume cha sheria kwa muda wa zaidi ya miaka 10 ambapo alilazimisha wanawake na wanaume kushiriki ngono muda mrefu, wakiwa wametumia dawa za kulevya.

Combs ambaye amekuwa akizuiliwa katika gereza la Brooklyn kwa zaidi ya mwaka mmoja alikanusha mashtaka yote matano dhidi yake mbele ya mahakama.

Waamuzi hata hivyo walimwondolea kosa moja la kushirikiana na wengine kupanga uhalifu na mawili ya usafirishaji kwa ajili ya ngono, kulazimisha watu kushiriki ngono na ulaghai.

Website |  + posts
Share This Article