Bingwa wa Jumuiya ya Madola Ferdinand Omanyala na mshindi wa nishani ya fedha ya Olimpiki Kenny Bednarek wa Marekani watazindua uhasama katika fainali ya mita 100 ya makala ya tano ya mashindano ya Kip Keino Classic Continental Tour tarehe 20 mwezi huu katika uwanja wa Nyayo.
Bednarek atakuwa akishiriki Kip Keino Classic kwa mara ya tatu na ya pili mtawalia baada ya kumaliza wa pili nyuma ya Omanyala mwaka uliopita.
Mshindi wa nishani ya fedha ya dunia Letsile Tebogo wa Botswana atashiriki mita 200 sawa na mshindi wa nishani ya fedha ya Olimpiki Christine Mboma wa Namibia.
Kulingana na Mkurugenzi wa mashindano hayo Barnaba Korir matayarisho yote yamekamilika kwa makala ya mwaka huu yanayorejea uwanjani Nyayo kutokana na ukarabati unaoendelea Kasarani.
Korir amefichua kuwa Kenya tayari imeanza mikakati ya kuomba maandalizi ya mkondo mmoja wa Diamond League akielezea imani ya Kenya kufanikiwa katika agenda hiyo.
Mashindano ya Kip Keino Classic yatakuwa ya mkondo wa pili kati ya misururu 11 ya mwaka huu katika mashindano ya kiwango cha dhahabu na ni ya pili baada ya mkondo wa Melbourne ulioandaliwa Februari 15 mwaka huu.
Mkondo wa Kenya utakuwa na vitengo vya mashindano ya kitaifa,mashindano ya chama cha riadha na kitengo kikuu .
Kitengo kikuu kitashirikisha mita 100 kwa wanaume na wanawake,mita 200 wanaume,mita 400 kuruka viunzi,mita 800 kwa wanaume na wanawake na shindano la urushaji nyundo.