Omanyala kuongoza timu ya Kenya kwa mbio za Dunia za kupokezana kijiti

Kikosi cha Kenya kitaripoti kambini Jumanne ijayo kujiandaa kwa mashindano hayo ya Dunia ambayo pia yatakuwa ya kufuzu kwa mashindano ya Dunia ya Tokyo Septemba mwaka huu.

Dismas Otuke
2 Min Read

Bingwa wa Jumuiya ya Madola katika mbio za mita 100 Ferdinand Omanyala, ataongoza kikosi cha Kenya kwa makala ya 7 ya mbio za Dunia za kupokezana kijiti yatakayoandaliwa mjini Guangzhou, China, baina ya tarehe 10 na 11 mwezi ujao.

Chama cha riadha Kenya kimeteua kikosi cha wanariadha 21 kufuatia kukamilika kwa majaribio ya siku moja katika uwanja wa kitaifa wa Nyayo.

Omanyala amejumuishwa katika timu ya wanaume mita 100 kwa wanariadha wanne kupokezana kijiti, ambayo inamjumuisha kakake mdogo Isaac Omurwa, Meshack Babu, Mark Otieno, Steven Onyango na Moses Wasike.

Bingwa wa dunia wa mita 800 Mary Moraa amejumuishwa katika kikosi cha mita 400 kwa wanariadha wanne kupokezana kijiti pamoja na Mercy Adongo, Esther Mbagari, Mercy Chebet, Lanoline Owino, Vanice Kerubo, Gladys Mumbe na Hellen Syombua.

Bingwa wa mashindano ya wanajeshi mwaka jana Boniface Mweresa, ataonmgoza kikosi cha mita 400 kwa wanariadha wanne kupokezana kijiti pamoja na Kevin Kipkorir, Brian Tinega, Allan Kipyego, Kelvin Kiprotich, David Sanayek na Wiseman Were.

Kikosi cha Kenya kitaripoti kambini Jumanne ijayo kujiandaa kwa mashindano hayo ya Dunia ambayo pia yatakuwa ya kufuzu kwa mashindano ya Dunia ya Tokyo Septemba mwaka huu.

Kenya iatashiriki katika mbio za mita 100 kwa wanariadha wanne kupokezana kijiti wanaume, mita 400 kwa wanariadha wanne kupokezana kijiti kwa wanaume na wanawake, na mita 400 kwa wanariadha wanne jinsia mchanyato katika mbio za dunia za kupokezana kijiti mjini Guangzhou, China.

Website |  + posts
Share This Article