Askofu Mkuu wa Kanisa la Kianglikana nchini (ACK) Jackson Ole Sapit amepiga marufuku wanasiasa kuongea katika makanisa ya ACK kote nchini.
Ole Sapit amesema wanasiasa watauruhusiwa tu kuzungumza na waumini nje ya kanisa baada ya ibada.
Aidha, kasisi huyo amesema kanisa lake kamwe halitatangaza sadaka inayotolewa kanisani na waumini au washirika.
Ole Sapit ametangaza haya Jumapili wakati wa ibada iliyohudhuriwa na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua na kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka.
Miongoni mwa viongozi wengine waliohudhuria ibada hiyo ni Eugene Wamalwa wa chama cha DAP-K na Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja.
Kinyume cha matarajio yao, wote hao walinyimwa fursa ya kuwahutubia waumini na walitambulishwa tu kwa kutajwa majina.
Wanasiasa katika siku za hivi karibuni wamegeuza madhabahu kuwa majukwaa ya kupiga siasa, wakitumia majukwaa hayo kurushiana cheche za maneno bila kujali kuwa wapo mahali patakatifu.
Hata hivyo, kunayo makanisa ambayo kamwe huwa hayaruhusu wanasiasa kuwahutubia waumini kwenye madhabahu, na hatua ya ACK imepongezwa na Wakenya wengi kama itakayosaidia kuleta heshima makanisani.