Wizara ya Elimu imetoa hakikisho kwamba mitihani ya kidato cha nne (KCSE) iliyoratibiwa kufanywa siku ya Ijumaa, haitaathiriwa licha ya siku hiyo kutangazwa sikukuu ya taifa, kutoa nafasi ya kuapishwa kwa Prof. Kithure Kindiki kuwa Naibu Rais.
Kupitia kwa taarifa, Waziri wa Elimu Julius Migos Ogamba, amewaagiza wanachama wa asasi mbalimbali kuhusu usimamizi wa mitihani, kufika kazini jinsi ilivyoratibiwa awali.
“Wizara ya Elimu inafahamisha umma kuwa, kutangazwa kwa sikukuu ya taifa, hakutaathiri mitihani ya kidato cha nne, KCSE iliyoratibiwa kufanywa Ijumaa Novemba 1,2024,” ilisema taarifa hiyo.
“Wanachama wote wa asasi mbali mbali kuhusi usimamizi wa mitihani, wanagizwa kufika kazini kuhakikisha shughuli zote za mitihani zinatekelezwa kuambatana na miongozo ya wizara ya elimu.”
Aidha kulingana na taarifa hiyo, taasisi zingine za elimu ya msingi zinazoendelea na shughuli za masomo, zimetakiwa kufuatilia ratiba zao kuhakikisha zinatimiza kalenda ya masomo.