Waziri wa elimu Julius Ogamba, ameelezea kujitolea kwa serikali kukamilisha ujenzi wa madarasa ya gredi ya tisa kwa wakati.
Ogamba alisema ifikapo mwezi Januari mwaka ujao, madarasa hayo yatakuwa tayari kwa wanafunzi wa gredi ya tisa, ambao ndio waanzilishi wa mfumo mpya wa elimu wa CBC.
Akizungumza Ijumaa alipozindua madarasa mapya katika shule ya Kanyumbani kaunti ndogo ya Rabi, kaunti ya Kilifi, waziri huyo pia aliwaonya wale ambo wamenyakua ardhi ya shule kuwa chuma chao ki motoni.
Alisema wale ambao wamenyakua ardhi ya shule hawana budi kufidia kipindi ambacho wametumia ardhi hiyo.
Waziri wa elimu Julius Ogamba alisema wizara yake imegundua shule nyingi hapa nchini hazina hatimiliki au ardhi yao imenyakuliwa na walaghai.
Alidokeza kuwa kamati maalum ya ukaguzi wa hesabu imebuniwa, ili kukusanya deta ya mali ya shule ikiwemo ardhi katika harakati za maandalizi ya kupokea hatimiliki.
Ogamba pia alitoa wito kwa jamii zinazoishi karibu na shule kusaidia kuhifadhi ardhi inayomilikiwa na shule kwa ajili ya upanuzi wa siku zijazo.