ODM yapongeza uamuzi wa jopo la kutatua mizozo ya vyama vya kisiasa

Tom Mathinji
2 Min Read
Kiongozi wa chama cha ODM Oburu Oginga.

Chama cha  Orange Democratic Movement (ODM), leo Alhamisi kimepongeza uamuzi wa jopo la kutatua mizozo ya vyama vya kisiasa wa kutupilia mbali malalamishi yaliowasilishwa na Katibu Mkuu wa chama hicho,  Edwin Sifuna.

Uamuzi wa jopo hilo sasa unaipa chama hicho fursa ya kuandaa mkutano maalum wa wajumbe utakaofanyika siku ya Ijumaa.

Kupitia kwa taarifa iliyotiwa Saini na  Mkurugenzi wa Mawasiliano Philip Etale, chama hicho kilisema jopo hilo lilitupilia mbali kesi ya Sifuna kwa kukosa kuzingatia njia ya kutatua mizozo chamani, kikisisitiza kwamba chama hicho kina uwezo wa kutatua mizozo chamani.

“Katika kesi iliyowasilishwa na Seneta Edwin Sifuna, jopo hilo lilitupilia mbali kesi hiyo kwa kukosa kutumia mikakati ya kusuluhisha mizozo chamani,” ilisema taarifa hiyo.

Vile vile kwenye kesi iliyowasilishwa na Vincent Chepkwony, jopo hilo pia lilikataa kusimamisha kwa muda uamuzi wa Baraza Kuu la chama hicho (NEC), la Februari 11, 2026.

Chama cha ODM kimewaalika wajumbe walioteuliwa kuhudhuria mkutano maalum wa wajumbe unaotarajiwa kufanyika kwenye uwanja wa maonyesho ya kilimo wa Jamhuri jijini  Nairobi, Ijumaa saa tatu asubuhi.

Jopo la kusikiza kesi za  mizozo ya vyama vya kisiasa  lilimuagiza seneta wa  Nairobi Edwin Sifuna na chama cha ODM, kujaribu kutatua mizozo yao kuhusu kuondolewa kwake katika nafasi ya katibu mkuu wa chama hicho kupitia njia za kutatua mizozo za chama hicho.

Share This Article