Chama cha ODM kimelaani vikali hatua ya serikali kuzuia wanafunzi wa shule ya wasichana ya Butere kutoka kaunti ya Kakamega kuwasilisha mchezo wao wa kuigiza wenye kichwa “Echoes of War.”
Wanafunzi hao walitarajiwa kuigiza mchezo huo wakati wa Tamasha la Taifa la Michezo ya Kuigiza linalofanyika mjini Nakuru.
“Nchi imetazama kwa kutoamini, kisa cha kusikitisha kwenye Tamasha la Taifa la Michezo ya Kuigiza mjini Nakuru ambapo serikali imeonekana kutia baridi kutokana na mchezo wa kuigiza wa shule ya upili ya wasichana ya Butere wenye kichwa, ‘Echoes of War’,” alisema Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna kwenye taarifa.
“Masuala nyeti yanaibuka wakati serikali inapoogopa sanaa ya watoto, hali tu ya kunadi kipaji katika tamasha la shule ya upili,” aliongeza Sifuna ambaye pia ni Seneta wa kaunti ya Nairobi.
Chama hicho aidha kimelaani vikali kudhulumiwa kwa shule ya upili ya wasichana ya Butere, wanahabari na watu wengine waliohudhuria tamasha hilo na kushinikiza kuwa shule ya Butere ikubaliwe kuwasilisha mchezo wake wa kuigiza.
Awali, polisi waliripotiwa kuwafurusha wanafunzi wa shule ya wasichana ya Butere kutoka kwa Tamasha la Taifa la Michezo ya Kuigiza , linaloendelea katika ukumbi wa Melvin Jones, kaunti ya Nakuru.
Wanafunzi hao waliagizwa kuondoka ukumbini kutokana na mchezo wao wa kuigiza waliopanga kuwasilisha kwa kichwa “Echoes of War” kwa madai ya kuchochea uhasama.
Wanahabari na raia pia walizuiwa kuingia ukumbini kutazama tamasha hilo huku pia polisi wakifyatua vitoza machozi kuwatawanya wananchi waliotaka kuzua rabsha baada ya wanafunzi hao kufurushwa.
Mwenyekiti wa chama cha KANU, Gideon Moi, amekashifu serikali kwa kuwanyima wanafunzi hao fursa ya kutumia kipaji chao.