Odinga asema hali Sudan Kusini inahitaji mwingilio wa haraka wa kimataifa

Raila alisema ziara yake nchini humo kama mjumbe maalum wa Kenya wa kujaribu kutuliza hali, imeafikia utambuzi wa mbinu za kushughulikia hali hiyo.

Marion Bosire
2 Min Read
Raila Odinga, Kiongozi wa Upinzani

Waziri mkuu wa zamani wa Kenya Raila Odinga amesema kwamba hali nchini Sudan Kusini, inahitaji mwingilio wa haraka wa jamii ya kimataifa.

Akihutubiwa wanahabari jana Jumamosi, Raila alisema ziara yake nchini humo kama mjumbe maalum wa Kenya wa kujaribu kutuliza hali, imeafikia utambuzi wa mbinu za kushughulikia hali hiyo.

Haya yanajiri wakati uhusiano kati ya Rais Salva Kiir na mpinzani wake wa muda mrefu ambaye pia ni makamu wa kwanza wa Rais Riek Machar, unazidi kuharibika.

Alisema mazungumzo yake ya muda mrefu na Rais Kiir yalifichua kwamba Machar amewekwa katika kifungo cha nyumbani huku uchunguzi ukianzishwa kuhusu jinsi mgogoro wa hivi punde ulianza.

Mgogoro huo katika eneo la Nasir mwanzo wa mwezi huu wa Machi kati ya jeshi la Sudan Kusini – SSPDF na kundi liitwalo White Army uliongezeka na kusababisha mauaji ya mfanyakazi wa shirika la umoja wa mataifa na afisa mmoja mkuu wa jeshi.

Raila amesema kwamba ataandika ripoti kuhusu mawasiliano yake na Rais salva Kiir na mwelekeo ibuka wa kuafikia amani ya kudumu nchini Sudan Kusini.

Alipotoka Sudan Kusini, Raila alienda Entebbe, Uganda kwa mazungumzo na Rais Yoweri Museveni huku akidhihirisha imani kwamba amani inaweza kupatikana nchini Sudan Kusini.

Rais William Ruto alimteua Raila Odinga kuwa mjumbe maalum wa Kenya nchini Sudan Kusini hasa baada ya kuzuiliwa nyumbani kwa Riek Machar.

Website |  + posts
Share This Article