Aliyekuwa Rais wa Nigeria Olesegun Obasanjo amemuunga mkono Raila Amolo Odinga anapowania uenyekiti wa tume ya umoja wa Afrika AUC.
Wakati akizungumza katika ikulu ya Nairobi wakati wa uzinduzi rasmi wa uwaniaji wa Raila wa wadhifa huo, Obasanjo wa umri wa miaka 87 alisema kwamba Raila anatosha kwa wadhifa anaosaka kutokana na tajriba yake.
Rais huyo wa zamani wa Nigeria aliorodhesha matatizo yanayokumba bara Afrika kama vile ukosefu wa uthabiti, usalama, umasikini na mengine akisema kwamba yanahitaji kiongozi anayeweza kuyashughulikia.
Kuhusu hati ya Visa ya bara Afrika aliyoitaja Raila kama mojawapo ya malengo yake, Obasanjo alisema kwamba anasubiri kwa hamu ujio wa hati hiyo punde baada ya Raila kuanza kuhudumu kama mwenyekiti wa AUC.
Hii ni ishara ya imani aliyonayo kiongozi huyo kwamba Raila ataibuka mshindi wa kinyang’anyiro cha uenyekiti wa AUC.
Aliongeza kwamba awali, amejipata pagumu pale anapoalikwa kwenye nchi fulani barani Afrika lakini anakosa kwenda kwa sababu ya kushindwa kupata Visa za nchi hizo.
Kabla ya kuanza hotuba yake hata hivyo, Obasanjo aliwachekesha waliokuwepo pale ambapo aling’ang’ana kuondoa kibao alichokuwa amewekewa asimamie ili aweze kufikia kipaaza sauti.
Kwanza alijaribu kukisukuma kando kwa kutumia mguu wake lakini hakuweza na akainama akakiondoa kwa mkono.
Baada ya kufanikiwa alimtania aliyekiweka kibao hicho akisema, “Mimi sio mfupi mnavyodhania.”
Alisema ana imani kwamba kumfahamu Raila kumekuwa baraka kwa maisha yake na kwamba ataifanya Afrika iwe yenye uwezo, yenye amani na yenye mafanikio.
Uchaguzi wa mwenyekiti wa tume ya umoja wa Afrika utaandaliwa mwezi Februari mwaka ujao ambapo mrithi wa Moussa Faki Mahamat wa Chad atakuwa anasakwa kati ya wawaniaji wanne.
Kando na Raila wawaniaji wengine ni Anil Gayan wa Mauritius, Mahmood Ali Youssof wa Djibouti na Richard Randriamandrato wa Madagascar.
Viongozi wa nchi wanachama wa umoja wa Afrika ndio watapiga kura kuchagua mwenyekiti wa AUC na kura itakuwa ya siri.