Mshawishi wa mitandao ya kijamii nchini Iraq Om Fahad ameuawa kwa kupigwa risasi nje ya nyumba yake mjini Baghdad, kulingana na ripoti za vyombo vya habari.
Shambulio hilo lilitokea katika kitongoji cha mji mkuu wa Zayne mashariki mwa mji huo siku ya Ijumaa.
Wizara ya mambo ya ndani ya Iraq ilithibitisha katika taarifa kwamba “mwanamke maarufu katikae mitandao ya kijamii” ameuawa na “washambuliaji wasiojulikana”.
Iliongeza kuwa “timu maalum” imeundwa kuchunguza mazingira ya kifo chake.
Fahad, ambaye jina lake halisi ni Ghufran Sawadi, aliripotiwa kupigwa risasi ndani ya gari lake na mtu aliyekuwa na bunduki akiendesha pikipiki.
Chanzo cha usalama cha Iraq kililiambia shirika la habari la AFP kwamba mshambuliaji huyo alionekana kujifanya kuwa analeta chakula.
Shirika la habari la Al Hurra linalomilikiwa na Marekani, wakati huo huo, liliripoti kuwa mwanamke mwingine alijeruhiwa katika shambulio hilo.
Fahad alijulikana sana kwenye TikTok kwa kushiriki video zake akicheza hadi muziki wa pop akiwa amevalia mavazi ya kubana – na kujipatia maelfu ya wafuasi.
Alihukumiwa kifungo cha miezi sita gerezani kwa kushiriki video ambazo mahakama iliamua zinadhoofisha “maadili ya umma”.