Ana da Silva Miguel maarufu mitandaoni kama Neth Nahara raia wa Angola, amehukumiwa kifungo cha miaka miwili gerezani kwa kosa la kumtukana Rais wa nchi hiyo, João Lourenço.
Inaripotiwa kwamba nyota huyo wa mtandao wa TikTok alimlaumu Rais Lourenço kwa vurugu na ukosefu wa mpangilio. Aliongeza kwamba Rais ndiye wa kulaumiwa kwa ukosefu wa shule, nyumba za makazi na fursa za ajira.
Mnamo mwezi Agosti mwaka huu, mahakama ilimhukumu Neth Nahara kifungo cha miezi 6 gerezani, hukumu ambayo ilipingwa katika mahakama ya rufaa na kifungo kuongezwa hadi miaka miwili.
Waliowasilisha rufaa hiyo walisema adhabu ya kifungo cha miezi sita gerezani ilikuwa nyepesi mno ikilinganishwa na kosa lake.
Neth Nahara alikuwa ameomba mahakama impatie adhabu nyepesi kwa sababu hayo ndiyo makosa yake ya kwanza na kwamba ni mama ya watoto wa umri mdogo, ombi ambalo lilikataliwa na mahakama.
Mahakama iliamuru kwamba Neth amlipe Rais Lourenço dola 1,200 kwa kumharibia jina.
Jaji Salomão Raimundo Kulanda alimtaja Rais Lourenço kuwa kiongozi huru.
Katika mtandao wa TikTok, Miguel ana zaidi ya wafuasi 230,000 na video zake hutizamwa na wengi.
Wakili wake alisema hiyo ndiyo mara ya kwanza kwa mtu kuhukumiwa nchini humo kutokana na walichochapisha kwenye TikTok.